RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein leo ametembelea miradi ya Maendeleo ukiwemo mradi wa gati
mpya pamoja na mradi wa maji safi na salama huko Wilaya ndogo Tumbatu Mkoa wa
Kaskazini Unguja na kueleza kuwa ahadi zake zina lengo la kuwasaidia wananchi
na kuwaletea maendeleo endelevu.
Akizungumza na
wananchi mara baada ya kutembelea miradi hiyo Dk. Shein alisema kuwa amefurahishwa
kwa kiasi kikubwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo ambayo
itakuwa ni mkombozi mkubwa katika kuwaletea maendeleo sambamba na kuimarisha
huduma za kijamii.
Dk. Shein alisema
kuwa ujenzi wa gati mpya umejengwa kwa kitaalamu zaidi kwani gati hiyo
itahilimi vishindo vya vyombo vyote kwani juhudi hizo zote ni kwa ajili ya
usafiri wa uhakika wa wananchi wa kisiwa cha Tumbatu pamoja na bidhaa zao hasa
ikizingatiwa kuwa wananchi hao wa Tumbatu wao wenyewe ndio waliokuwa mafundi
chini ya usimamizi wa Shirika la Bandari.
Katika maelezo
yake Dk. Shein alisema kuwa ujenzi huo
wa gati ni miongoni mwa maendeleo makubwa yaliokusudiwa kwa ajili ya wananachi
wa Tumbatu ambapo kabla ya kuwepo kwa gati hiyo wananchi hao walikuwa wakipata
usumbufu mkubwa.
Akieleza kuhusu mradi
mpya wa maji safi na salama, Dk. Shein
alisema kuwa kutokana na kuwa maji ni uhai na hakuna maisha ya mwanaadamu bila
ya kuwepo kwa huduma ya maji ndipo Serikali ikaona haja ya kuwaongeza huduma
hiyo wananchi wa Tumbatu kwa kuanzisha mradi huo mpya wa maji.
Dk. Shein alisema kuwa
lengo na madhumuni ya mradi huo ni kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wa
Tumbatu hivyo aliwataka wananchi hao kuutunza mradi huo ili uwasaidie zaidi wao
na vizazi vyao vijavyo.
Aidha, Dk. Shein
aliwaahidi wananchi wa Tumbatu kuwa matangi kwa ajili ya maji yatajengwa kisiwani humo na Serikali kwani uwezo huo
inayo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliwataka wananchi wa Tumbatu kuwapuuza wale wote watakaobeza miradi hiyo
kwani hulka hizo ni miongoni mwa hulka za baadhi ya wanaadamu na kusisitiza
kuwa mwanaadamu yeyote anaepata neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu ni vizuri
akashukuru.
Dk. Shein pia,
alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Tumbatu kwa kushiriki vyema katika
ujenzi wa miradi hiyo na kuwaadi kuwa Serikali yao itaendelea kuwaunga mkono
katika kuwapelekea miradi ya maendeleo.
Akitoa shukurani kwa
wazee wa Tumbatu, Dk. Shein alipokea ombi lao la kutaka kuimarishiwa zaidi
kituo chao cha Polisi kwa lengo la kuongezewa ulinzi wanachi hao pamoja na mali
zao huku akiwaahidi kuwa juhudi zitachukuliwa na Serikali katika kukiimarisha
zaidi kisiwa cha Tumbatu kwa kujenga barabara pamoja na taa maalum za muangaza
wa jua kwa mashirikiano ya pamoja Serikali na uongozi wa Jimbo hilo.
Nae Mwakilishi wa
Jimbo la Tumbatu Mhe. Haji Omar Kheir alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi
zake za makusudi za kuhakikisha wananchi wa Tumbatu wanapata huduma bora
maendeleo zikiwemo huduma za afya, maji safi na salama,umeme, elimu ujenzi wa
gati na huduma nyenginezo.
Aidha, Mwakilishi huyo
wa Tumbatu ambaye pia, ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara
Maalum za SMZ alitoa pongezi kwa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pamoja na Wizara ya
Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kwa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM.
Mapema Mkurugenzi Mkuu
wa Bandari ya Zanzibar Abdalla Juma alimueleza Dk. Shein kuwa ujenzi wa gati
hiyo mpya ni kutekeleza agizo la Serikali na kusema kuwa kwa upande wa Tumbatu
umekamilika na kilichobaki ni mambo madogo madogo huku akieleza kuwa kwa upande
wa gati ya Mkokotoni ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwaka ujao.
Mkurugenzi Juma
alisema kuwa ujenzi wa gati hiyo mpya kwa upande wa Tumbatu ambayo tayari imeshaanza
kutumika hadi kumaliza kwake utagharimu Shilingi 374 ambapo kwa upande wa gati
ya Mkokotoni ambayo tayari michoro yake ipo, itagharimu zaidi ya Shilingi
Bilioni moja na wakati wowote tenda yake itatangazwa.
Alisema kuwa kwa upande
wa gati ya Tumbatu ni kwa ajili ya vyombo yote vidogo vidogo vikiwemo vile vya
kienyeji ambapo pia, limejengwa eneo maalum kwa ajili ya mizigo na kwa upande
wa Mkokotoni bandari hiyo mpya itatumiwa na hata boti kubwa.
Nae Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) Dk. Mustafa Ali Garu kwa upande wake alisema
kuwa mradi huo mpya wa maji safi na salama kisiwani unaotekelezwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar umeshaanza kutoa huduma huku akieleza kuwa mchango
mkubwa umetolewa na wananchi wa Tumbatu, Mwakilishi wa pamoja na Washirika wa
Maendeleo wakiwemo Ubalozi wa Marekani na Iran.
Garu alisema kuwa
mradi huo unatarajiwa kuwa na visima vitatu ambapo tayari hivi sasa kisima
kimoja kimeshaanza kazi kilichochimbwa huko Donge Kipange na vyengine
vinaendelea na kueleza kuwa kukamilika kwa visima hivyo na kuunganishwa kwake kutaondosha
kabisa upatikanaji wa maji kwa mgao kama ilivyo hivi sasa na badala yake
yatapatikana kwa muda wote wa masaa 24.
Garu alisema kuwa Mradi
huo unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia ZAWA ikiwa ni
pamoja na kulaza mabomba baharini na
uchimbaji visima na kueleza kuwa gharama za Mradi huo ni T. Shilingi
Bilioni moja na nusu na kwa hivi sasa tayari Shilingi milioni 700
zimeshatumika.
Nao wazee wa Tumbatu
walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa juhudi za makususdi anazozichukuwa za
kuwapelekea maendeleo wananchi wa kisiwa hicho sambamba na kutekeleza kwa
vitendo ahadi anazowaahidi.
Sambamba na hayo, Wazee
hao walimueleza Dk. Shein kuwasaidia kukiimarisha kituo chao cha polisi kwa
lengo la kuimarisha hali ya usalama katika kisiwa chao.
No comments:
Post a Comment