Wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar
wamehimizwa kuwa tayari kufanya kazi popote watakapopangiwa ambapo
watakuwa na wajibu wa kuthamini na kuchangia jitihada zinazoendelea kuchukuliwa
na Serikali katika kupambana na maradhi mbali mbali yanayoisumbua jamii Nchini.
Himizo hilo limetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein kwenye Mahafali ya 22 ya Chuo cha
Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar yaliyofanyika kwenye Kampas ya chuo hicho
yaliyopo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Jumla ya wahitimu 440 wa kada saba walihitimu na kufanikiwa
kupata stashahada mwaka huu wa masomo kukiwa na ongezeko kubwa mara mbili
ikilinganishwa na wahitimu 280 wa mwaka 2014.
Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohammed Shein ambae Hotuba yake
ilisomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Idii alisema wapo baadhi ya baadhi ya wahitimu wanaoajiriwa na Wizara ya Afya
wanapiga chenga kufanya kazi Kisiwani Pemba wakisahau kwamba Wananchi wa kisiwa
hicho wanahitaji kupata huduma zao.
Alisema watumishi wa Umma wakiwemo wa sekta ya afya
wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi na
miongozo ya sehemu wanazoajiriwa na inapendeza zaidi wawe mfano wa tabia njema
kwa kushikamana katika kutekeleza maadili ya kazi zao.
“ Nimefurahi kusikia kuwa katika orodha ya wahitimu wetu wa
fani za afya chuoni hapa wapo waliotoka Tumbatu, Kojani, Fundo, Mtende, na
Maeneo mengine ambayo watu wengi huwa wanaona tabu kwenda kufanya kazi kutokana
na mazingira ya Kijiografia yaliyopo “. Alisema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
aliiagiza Wizara ya Afya kufanya tathmini ya mahitaji ya wataalamu wa afya
katika maeneo hayo ili kujua changamoto zilizopo na hatua za haraka zichukuliwe
zitakazowezesha vijana kutoka maeneo hayo wanaajiriwa.
Alisisitiza kwamba Wizara ya Afya ihakikishe inaweka
utaratibu kwa lengo la kuwawezesha Vijana wanaopangiwa katika maeneo hayo
wanafanya kazi kwa kipindi ambacho Wizara itaona kinafaa bila ya kukiuka sheria
za mikataba ya kazi.
Akizungumzia suala la uwekezaji katika sekta ya Afya Nchini
Rais wa Zanzibar alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikishajiisha
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika sekta hiyo muhimu jambo
ambalo limekuwa likisaidia sana katika kuimarisha huduma za afya Nchini.
Alisema juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha
huduma za afya kwa kushirikiana na wawekezaji na washirika wa maendeleo
zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza pia soko la ajira hasa kwa wahitimu wa
Chuo hicho.
“ Mwezi Machi mwaka huu nilialikwa kuifungua Hospitali ya
Tasakhtaa inayoendeshwa na Global Hospitals ya India katika Mtaa wa Vuga. Hii
ni Hospitali ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kutibu maradhi mbali mbali “.
Alisisitiza Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar aliwasisitiza wahitimu wa Chuo cha Taaluma
za Sayansi za Afya Zanzibar kuchangamkia ajira zinazotolewa na Serikali na
Sekta Binafsi wakitambua kwamba Hospitali zote zina lengo la kuimarisha huduma
za afya kwa faida ya Wananchi.
Kuhusu upatikanaji wa ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa
taasisi za umma Rais Shein alisema changamoto kubwa ya mahitaji ya Serikali
zinasababisha ruzuku hizo kutofikia kiwango halisi kinachoweza kuridhisha
taasisi hizo.
Hata hivyo Rais wa Zanzibar aliiagiza Wizara ya afya pamoja
na Wizara ya Fedha Zanzibar kufanya mapitio ya ruzuku inayopewa Chuo cha
Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar.
Alieleza kwamba endapo ikithibitika kuwa kiwango
kinachotolewa ni kidogo, uwe9o mjadala na kuangaliwa utaratibu wa namna ya
kuweza kuwaongezea ili chuo hichi muhimu kiweze kuendesha mipango ya maendeleo
kinachijipangia.
Aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya
Zanzibar kwa kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali
tokea kilipoanzishwa katika kuimarisha sekta ya afya kwa misingi iliyowekwa na
waasisi wa Afro Shirazy Party wakati wa kupigania uhuru wa Nchi hii.
Alisema chuo hicho hivi sasa kimekuwa chem chem ya kutoa
wataalamu mbali mbali wanaohitajika katika Hospitali na Vituo tofauti vya Afya
hapa Nchini kwa lengo la kuwapatia Wananchi huduma bora za Afya.
Alieleza kwamba Taifa kwa sasa limepiga hatua kubwa kwa
kusomesha wataalamu wazalendo wenyewe jambo ambalo limesaidia kuokoa fedha
nyingi ambazo zingelazimu kulipa kwa ajili ya kuwasomesha wataalamu hao nje ya
Nchi kama ilivyokuwa ikifanywa hapo zamani.
Mmoja wa wahitimu hao Faika Karim Zam kwa niaba ya
wenzake wameuomba Uongozi wa Chuo hicho kuanzisha mafunzo ya ngazi ya Shahada {
Diploma } kwa nia ya kuwapunguzia gharama za kutafuta elimu hiyo nje ya nchi.
Faika Karim alisema uanzishwaji wa mafunzo hayo ni vyema
ukaenda sambamba na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia, huduma za
Maktaba,kukabiliana na upungufu wa Walimu wa kudumu na watakuwa tayari
kuusaidia Uongozi huo ili wanafunzi wanaofuatia wafaidike na Mpango huo.
Alifahamisha kwamba hatua hiyo itawawezesha wanafunzi
wanaoingia kwenye Chuo hicho muhimu kupata taaluma ya kisasa inayokwenda
sambamba na mabadiliko ya dunia yaliyopo hivi sasa ya sayansi na Teknolojia.
Mapema Mkuu wa Chuo cha Taalum za Sayansi za Afya Zanzibar
Dr. Haji Mwita Haji alisema Uongozi wa Chuo hicho kupitia Baraza lake umeamua
kuongeza majengo zaidi ili kuwahudumia vyema wanafunzi wanaoamua kujiunga na
chuo hicho sambamba na mahitaji ya ongezeko la Hospitali na vituo vya Afya
Nchini.
Dr. Mwita alisema hatua hiyo inalenga kukijengea hadhi na
sifa chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1938 kikiwa miongoni mwa vyuo vichache
barani Afrika vilivyokuwa vikitoa elimu ya Afya licha ya kwamba hakikuwa na
makaazi ya Kudumu.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kushirikiana na Serikali ya Oman kwa muono wao wa kuenga majengo ya kudumu ya
chuo hicho ambayo yanatoa fursa kwa Chuo hicho katika muelekeo wake wa
matayarisho ya kuwa kitengo cha Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA }.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufungaji wa Mahafali hayo
ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar, Naibu Waziri wa Afya
Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo aliwaomba wauguzi kufuata maadili
ya kazi zao ili kupunguza au kuondosha kabisa malalamiko yanayotolewa na
wananchi.
Mh. Mahmoud alisema lugha zao kwa wagonjwa ndio kitendo
kilichompa wakati mgumu alipokuwa akijibu maswala ya wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi katika Vikao vya Baraza hilo vilivyokuwa vikiendelea kwa muda wote
wa miaka mitano iliyopita.
Naibu Waziri wa Afya aliwapongeza Wafanyakazi wa Sekta
ya Afya wa muda mrefu walioamua kujisajili na kupata taaluma na hatimae
kufanikiwa kuwa miongoni mwa wahitimu wa mkupuo wa 22 wa Chuo cha Taaluma za
Sayansi za Afya Zanzibar.
Alisema Watendaji wote kwa sasa wanapaswa kubadilika kwenda
na wakati unaokwenda sambamba na teknolojia ya kisasa ya sayansi iliyopo
ulimwenguni ambayo humuwezesha mfanyakazi kufanya kazi mahali popote Duniani.
Wahitimu 440 wamefanikiwa kupata stashahada katika fani saba
za sekta ya afya ambazo ni pamoja na Afisa Tabibu wa Afya ya Kinywa na Meno,
Afisa Tabibu, Afya ya Maingira, Uuguzi na Ukunga, Utabibu wa Maabara,Madawa
pamoja na Ufundi Sanifu wa Vifaa vya Hospitali.
Katika Mahafali hayo ya 22 ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za
Afya Mgeni rasmi pia alifanikiwa kutoa vyeti Maalum kwa Wanafunzi bora zaidi wa
kila fani katika mafunzo hayo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment