NA KABUGA KANYEGERI
MAMBO 10 AMBAYO MKE MWEMA HAFANYI
Ni matumaini yangu kuwa ulisoma mada iliyopita juu ya “dondoo 10 zinazochangamsha ukaribu wenu wa kimapenzi”, na ni imani yangu kuwa imesaidia katika kuboresha ndoa yako.
Kama ni hivyo basi, leo tena ninakuletea kitu kizuri chenye manufaa katika kuboresha ndoa yako na kuifanya kuwa maridhawa.
Kama wataka kuwa na ndoa yenye furaha jiweke mbali na tabia hizi mbaya ambazo zitakufanya uwe mke mwenye kuogofya sana.
Hapa nimekuwekea orodha ya mambo 10 mabaya ambayo unaweza ukawa unamfanyia mumeo na yakawa hayana msaada wowote kwenye ndoa yako:
1. Usumbufu
Amini usiamini, mumeo ni mtu mzuri na maridadi sana. Nakwambia kweli, ni mtu maridhawa. Mara nyingi anasikiliza unachosema, anaelewa kinachotakiwa kufanyika, na mara nyingi anakuwa na nia ya dhati ya kufuata hicho unachokitaka. Lakini, atakifanya kwa muda wake na kwa njia anayoiona yeye, na hata ufanye usumbufu kwa kiwango gani huwezi kuibadilisha hiyo. Usumbufu utazidisha mvutano.
2. Kulalamika
Maisha yenu yanaweza yasiwe mazuri sana, lakini kulalamika kuhusu maisha hayo hakuwezi kuyafanya yawe mazuri. Naam, ni muhimu umshirikishe mumeo vitu ambavyo unahisi kama vinakuudhi, ambavyo vinakutibua na kukuchanganya au kukuhuzunisha. Lakini, hakikisha kuwa mambo hayo hayawi mambo pekee unayomwambia. Malalamiko endelevu na mtazamao hasi unaweza kutawala na kutamalaki uhusiano wenu. Hivyo, jaribu kuwa na mtazamo chanya na kufanya vitu chanya.
3. Udhalilishaji au Umbea
Bila shaka wewe na marafiki zako mnapenda kukaa pamoja na kuzungumzia kila kitu kinachopatikana chini ya jua. Lakini, wakati mwingine mazungumzo yenu hayo huenda mbali sana. Marafiki zako wanaweza wakataka kujua kila kitu kuhusu maisha yako binafsi, lakini hilo si jambo zuri. Usimfanyie hila mumeo mbele ya marafiki zako, hata kama wao wanawafanyia hila waume zao. Usijaribu kumkosoa mbele ya watu. Kama kuna mambo yanatakiwa kushughulikiwa, basi tafuta muda mzuri mnapoweza kuzungumza na kuyashughulikia kwa pamoja – wewe na mumeo tu.
4. Kukosa heshima
Waume wengi sio wakamilifu, na wengi wao wanalijua hilo. Licha ya mapungufu yao, inaonekana kuwa wanaume wengi hukubali kurekebishwa pindi urekebishaji na ukosoaji huo unapofanyika katika njia ya upendo na yenye nia ya kujenga – wanachotaka wao ni kuona kuwa wanaheshimiwa wakati wa kuwarekebisha. Kuna namna nyingi unaweza ukawa unamvunjia heshima na adabu mumeo kwa kujua au kwa kutojua. Miongoni mwa njia hizo ni pamoja na kuendelea kumkatisha anapokuwa akizungumza, kutomshauri katika kufanya maamuzi muhimu, au kubadilisha maamuzi yake.
5. Kuwapa kipaumbele watu wengine
Ninafahamu kuwa labda umetingwa na kazi. Unaweza ukawa na majukumu ya kazi, watoto, na mazungumzo na marafiki zako. Kila mtu anaweza kuona kuwa wewe ni mwanamke mchapazi – isipokuwa mume wako. Anaweza kuhisi kuwa amepuuzwa. Tafadhali usimsahau kwa kuwaweka watu wengine au vitu vingine mbele yake. Anahitaji kujua kwamba yeye ndio kipaumbele chako namba moja.
6. Kumnyima jimai
Tendo la ndoa halipaswi kuwa kama kitu cha kubembelezea. Kufanya hivyo kunalifanya tendo hilo kuwa kitu kisichokuwa na thamani. Linapaswa kuwa nyenzo ya kuwaunganisha na kuwaweka karibu zaidi. Usilitumie kama nyenzo ya kumdhibiti mume. Tendo la ndoa ni ndoa yako. Mahitaji yako ya tendo la ndoa yanaweza kutofautiana na mahitaji yake, lakini hiyo haina maana ulichukulie kama peremende unayompa mwanao kwa kuwa mtoto mwema. Kama kuna kitu kinakuzuia kumpatia haki hiyo, basi jadiliana naye kuhusu tatizo hilo na mtafute suluhisho kwa pamoja.
7. Matumizi ya pesa kupita kiwango
Ninatambua kuwa hali za kiuchumi za wanandoa zinatofautiana, lakini ni ukweli kwamba masuala ya pesa yamekuwa chanzo cha migogoro ya ndoa nyingi na hata talaka nyingi. Iwapo wewe na mumeo hamtaafikiana katika masuala ya kifedha na kiuchumi, migogoro na mivutano inaweza ikazidi na hata kushindwa kuidhibiti.
8. Kuwa kama Mama yake
Mume wako ni mtu mzima, ingawa anaweza asionekane hivyo, na hajakuoa uwe mama yake wa pili. Sasa usijiweke katika nafasi ya mama yake. Badala yake, jitahidi uwe rafiki yake mpenzi na mtu ambaye anaweza akamuamini na kumpa siri zake. Pambana na tabia ya kukumuendesha, kumkaripia kwa kila analofanya au kumuamulia mambo yake. Ukimuacha azungumze na kukushirikisha mambo yake kwa njia anayoiona yeye ni bora kuliko kujaribu kumpeleleza au kudukiza taarifa zake.
9. Kuwa na matarajio yasiyokuwa na uhalisia
Mumeo anakupenda sana. Anataka kufanikisha mambo mazuri ambayo hata yumkini usingeyatarajia. Lakini, wakati fulani matarajio yanaweza kuwa makubwa na yasiweze kufikiwa. Anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya maajabu, lakini hata mtu wa aina hiyo uwezo wake una kikomo. Sikwambii kwamba ushushe kiwango cha hayo matarajio yako, lakini kumbuka tu kwamba baadhi ya vitu huchukua muda kukamilika, na huna sababu ya kuchanganyikiwa unapoona kuwa maendeleo yenu yanaenda taratibu. Waume wengi huona kuwa presha wanaoipata kutoka kwa waajiri, majirani au wakwe ni bora kuliko presha hiyo itoke kwa wake zao.
10. Kuchukua nafasi yake
Wanaume wanayapenda majukumu yao yanayowahusu. Huwafanya wajihisi kuwa wana nguvu. Jaribu kufikiria mumeo atakavyojisikia utakapotwaa mamlaka na madara yake. Anaweza kuhisi kuwa anapingwa na kuwa mwenye mtazamo wa kujilinda. Pamoja na mgawanyo wa majukumu katika ndoa yenu, muache mumeo awe mume, awe baba, kiongozi wa familia na kutekeleza majukumu yake. Usinyakue mamlaka yake. Anapotekeleza kazi yake vizuri mpongeze na umshukuru pia.
Ninatambua kuwa ndoa ina mambo mengi sana. Lakini ukiachana na tabia hizi mbaya na badala yake ukawa na matendo mazuri, unaweza kufurahia raha isiyokuwa na kikomo kutokana na ndoa yako kuwa maridhawa.
Ni matumaini yangu kuwa somo hili litakuwa na faida kwako itakayoongeza furaha tele!
Ungana nami katika mada ijayo…
NDOA MARIDHAWA GROUP..
WhatsApp: +255 763 348 213
No comments:
Post a Comment