PEMBA
WANAUSHIRIKA wa kikundi cha utengenezaji chumvi ‘Kibwekitu’,
kiliopo Kambini Kichokochwe Wilaya ya Wete Pemba, wameiomba serikali na taasisi
binafsi, kuwasaidia kwa kuwajengea kuta za saruji, ili kuzuia maji kuingia
katika mabwawa yao.
Walisema kuwa, wamekuwa na mabwawa yaliyojegwa kwa udongo,
jambo ambalo limekuwa ni tatizo kwao, kwani inaponyesha mvua hubomoka na
hatimae maji kuingia ndani yake.
Wakizungumza na mwandishi wa habari katika mashamba yao,
wanaushirika hao walisema, hali hiyo inawarudisha nyuma kimaendeleo, kutokana
na maji hayo kuharibu chumvi yote wakati yanapoingia.
Walisema, iwapo watajengewa mabwawa yao kwa kuta za saruji,
wataweza kuzalisha vizuri na kuweza kupata kipato kitakachoweza kuwakwamua na
umasikini.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Fatma Kombo Hamad alisema kuwa,
wamekuwa wakijipatia kipato kizuri iwapo chumvi yao haikuingia maji kwenye
mabwawa yao, jambo ambalo linawapa faraja ya kuendelea na kilimo chao hicho.
“Kipindi cha jua tunavuna vizuri, lakini ikitokezea mvua
katikati ya kilimo chetu huwa tunapata hasara, kwani dongo lote huporomoka na
na maji huingia ndani na kupelekea kuyeyuka”, alisema Mwenyekiti huyo.
Nae Katibu wa ushirika huo Said Suleiman Ali, alisema pia
wanahitaji mashine ya kusagia chumvi, ili waweze kukuza soko lao kwa kimataifa
zaidi.
“Iwapo tutapata mashine ya kusagia chumvi, tutakuza uchumi
wetu kwani tutakuwa na kiwanda na kuweza kuuza na soko la ndani na nje ya
nchi”, alisema.
Kwa upande wake mjumbe wa kikundi hicho, Maryam Salum Juma,
mafanikio ni mazuri wanayoyapata iwapo chumvi haikuingia maji, kwani wamepata
kujikwamua na hali mbaya ya umasikini kwa kiasi.
Nae Mshikafedha wa kikundi hicho, Bimkubwa Mussa Maalim
alisema soko ni zuri kwa upande wao, kwani kipolo kimoja hufikia shilingi
10,000 kwa baadhi ya nyakati.
“Kwa kweli soko ni zuri kiasi, lakini inategemea wakati
mwengine linashuka tunauza kipolo kimoja cha chumvi shilingi 6,000 mpaka elfu
8,000”, alifahamisha Mshikafedha huyo.
Alieleza kuwa, hutoka watu sehemu mbali mbali na kwenda
katika kikundi hicho kununua kwa jumla, jambo ambalo linawapa faraja kubwa ya
kuendelea na ushirika wao huo.
“Mwanzo ilikuwa tunatafuta watu wa kuwauzia, tunakodi gari
na kwenda sehemu mbali mbali, lakini kwa sasa Alhamdulillah watu wanatufuata
huku huku”, alisema.
Hadia Hamad Juma ambaye pia ni mjumbe wa kikundi hicho,
alisema kuwa lengo la kuanzisha kikundi hicho ni kujikwamua na hali ngumu ya
umasikini, ingawa bado wamekuwa na matatizo yanayowarudisha nyuma
Kikundi hicho cha Kibwekitu kimeanzishwa mwaka 2012, kikiwa
na wanachama 20 wakiwemo wanaume watano na wanawake 15, kinachojishughulisha na
utengenezaji wa chumvi ambapo changamoto yao kubwa ni mabwawa yao kubomoka na
kuingia maji, jambo ambalo ni hasara kubwa kwao.
sio kibwekitu ni kibwekiti
ReplyDelete