Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo (kushoto) akionyeshwa moja ya mipaka ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Zanzibar, katikati Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Zanzibar Mwalim Mbarouk Hamad na (kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Saleh Jidawi. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Msafara wa viongozi wa Mkoa Kusini Unguja na Wizara ya Afya wakitembelea eneo la Binguni lenye ukubwa wa ekari 80 linalotarajiwa kujengwa Hospitali ya rufaa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Zanzibar Mwalim Mbarouk Hamad akiwaonyesha viongozi wa Mkoa Kusini Unguja na Wizara ya Afya mchoro wa eneo lililopimwa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa Hospitali ya rufaa Zanzibar katika kijiji cha Binguni Wilaya ya Kati Unguja. Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Wananchi wanaoishi karibu na eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa katika kijiji cha Binguni, Wilaya ya Kati Unguja , wametakiwa kutolitumia eneo hilo kwa shughuli yeyote ya ujenzi ili kujiepusha na hasara inayoweza kuwapata.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Dkt. Idrissa Islam Hija ametoa ushauri huo wakati uongozi wa Wizara ya Afya ukiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mahmoud Thabit Kombo kufanya ziara ya kuliangalia eneo hilo ambapo imebainika baadhi ya wananchi wameanza kulivamia kwa ujenzi wa nyumba za kuishi.
Mkuu wa Mkoa amesema eneo hilo limepimwa rasmi kwa ajili ya matumzi ya Wizara ya Afya hivyo matumizi mengine yeyote yatakayofanywa hayatatambuliwa na uongozi wa Mkoa.
Katika hatua za awali za kulihifadhi eneo hilo, Dkt. Idrissa Islam Hija ameishauri Wizara ya Afya kuanza hatua ya kulizungushia uzio hatua kwa hatua ili wananchi wasipate mwanya wa kulivamia.
Amesema wananchi wamekuwa watukutu katika kufuata sheria za nchi na kila wanalofanya hudhani ni haki yao licha ya hatua za kuwaelimisha na kuwazuilia kuchukuliwa.
Aidha amewataka masheha na madiwani wa eneo hilo kutotowa vibali vinavyowaruhusu wananchi kujenga kwani uzoefu unaonyesha watu wanaovamizi maeneo kwa kujenga nyumba hupatiwa vibali na masheha ama madiwani.
“Madiwani na Masheha hamuruhusiki kutoa vibali vya matumizi ya ardhi na kufanya hivyo ni kosa jiepusheni na tabia hiyo hasa katika eneo hili lilitengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali,” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kati na Mkoa wa Kusini Unguja kuwazuiya wananchi wawili walioanza ujenzi katika eneo hilo na kuwataka wavunje nyumba hizo haraka iwezekanavyo.
Amesema iwapo watashindwa kuvunja majengo hayo wao wenyewe Wizara itasimamia kuvunja nyumba hizo na watalazimika kulipa gharama zote zitakazo .
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga eneo la ekari 80 katika kijiji cha Binguni kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Afya ambapo Wizara imeamua kulitumia kwa ajili ya kujenga Hospitali kubwa ya rufaa pamoja na nyumba za wafanyakazi
No comments:
Post a Comment