Na Pili Khatib na Zuhura Omar, MUM
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa
Zanzibar ZSTC Mwanahija Almas Ali amesema Maendeleo ya Sekta ya Zao la Karafuu
inaendelea kuimarika zaidi Zanzibar hasa baada ya kuanzishwa kwa Mfuko wa
Maendeleo ya Karafuu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya ZSTC
Maisara Bi. Mwanahija alisema Mfuko huo ulianzishwa kuongeza nguvu jitihada za
Serikali za kuimarisha zao hilo la uchumi wa Taifa.
Alisema utafiti ulifanyika juu ya namna ya kufanya mageuzi
yenye tija katika Sekta ya Karafuu ndipo ikaoneka umuhimu wa kuanzisha Mfuko
huo ambapo muda mfupi baada ya kuanzishwa unaonekana kuleta faida katika
uimarishaji wa zao hilo.
“Madhumuni ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu
ni kuhakikisha Sekta ya Karafuu inakua na kuimarika zaidi. Kuongeza idadi ya
mikarafuu na uzalishaji ambapo hivi sasa Wananchi wamehamasika zaidi katika
upandaji mikarafuu kwa wingi”. Alifahamisha Bi. Mwanahija.
Alisema Mfuko huo ambao upo chini ya Mkurugenzi Mwendeshaji
wa Shirika la ZSTC umejipanga kufanya sensa ya mikarafuu sambamba na kuwasajili
Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Aidha alifahamisha kuwa kupitia Mfuko huo na kwa
kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili kutafanyika tafiti kwenye kila
eneo linayohusu zao la karafuu kwa lengo la kugundua changamoto na kuzifanyia
kazi.
Alisema Shirika la ZSTC kwa kushirikiana na Wadau wengine
inakamilisha mpango maalumu wa kuziongezea hadhi na thamani karafuu za Zanzibar
kupitia mradi wa ‘Branding’ ili kuongezeka kwa uzalishaji kwenda sambamba na
kuongezeka kwa tija kwa Wakulima na Taifa.
Alisema hivi sasa mpango huo upo katika kutafuta vinasaba
vinavyoonyesha ubora wa karafuu za Zanzibar kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali
Zanzibar.
Alisema kupitia Mfuko huo Shirika limeongeza jitihada za
kutoa elimu kwa Wakulima juu ya uchumaji na uanikaji unaotakiwa ili kulinda
ubora wa zao hilo katika soko la nje.
Alisema Mfuko huo umekuwa ni msaada mkubwa katika
uimarishaji wa zao la karafuu hasa kwa Wakulima ambapo unatoa fidia kwa
Wakulima wanaopata ajali wakati wa uchumaji kupitia Shirika la Bima Zanzibar.
Alifahamisha kuwa Mfuko huo umelipa bima ya milioni 60 kwa
Shirika la Bima ili kuwafidia Wakulima 100 wanaokisiwa kupata ajali katika
zoezi la uchumaji wa karafuu mwaka 2015/2016 ambapo hadi sasa tayari watu tisa
wameripotiwa kupata ajali wote kutoka Pemba.
Alisema Wakulima wanaendelea kupata mikopo ya uchumaji
kupitia Mfuko huo na alifahamisha kuwa katika bajeti ya 2015/2016 Mfuko
umepanga kutumia milio 140 kwa ujenzi wa barabara ya Ng’omeni ikiwa ni msaada
wa kusadia miundombinu ya sehemu za uzalishaji wa karafuu.
Akizungumzia makadirio ya mavuno ya karafuu ya mwaka
2015/2016 Mkurugenzi huyo alisema Shirika limekadiria kununua tani 2800 mpaka
3200 katika mwaka huo.
No comments:
Post a Comment