PEMBA.
JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, limesema litaendelea
kushirikiana na waandishi wa habari kisiwani Pemba, kwa kutoa habari mbali
mbali ambazo jamii inatakiwa ifahamishwe.
Jeshi hilo limesema linamambo mengi ambayo yanatakiwa
kuandikiwa makala za Uchambuzi ambayo jamii haiyafahamu, ikiwemo masuaala ya
Utii wa sheria bila ya kushurutishwa.
Kauli hiyo imetolewa na kamanda wa Polisi Mkoa wa kusini
Pemba, Sheikhan Mohammed Sheikhan, wakati alipokuwa akifungua mafunzo ya siku
nne ya uwandishi wa makala kwa waandishi wa habari kisiwani Pemba,
yaliyoandaliwa na Pemba Press Club kwa Ufadhili wa UTPC, huko katika ukumbi wa
ZAC Chake Chake Pemba.
Alisema fani ya uandishi wa habari ni fani muhimu sana
katika kujenga uelewa kwa wananchi katika matukio mbali mbali ya kijamii,
kitaifa na hata kimataifa.
“Natambua Mchango wa Tasnia ya Uandishi wa habari katika
kuchapuza mauala mbali mbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, nawaombeni mutumie
kalamu zenu vizuri katika kuelimisha jamii”alisema.
Aidha aliwakumbusha waandishi wa habari kwamba habari
inaweza kuwa ni silaha ya kupelekea neema au kupeleka maafa katika jamii,
itegemea jinsi habari zitakavyotumika vizuri katika kuhimiza mambo ya manufaa.
“Habari yako inawezekana ikawa ni moja ya kuchochea
maendeleo kwa wananchi, lakini ukiutumia vibaya itakuwa ni chanzo cha Vurugu
jambo ambalo halikubaliki”alisema.
Hata hivyo kamanda Sheikhan aliwataka waandishi wa habari
kisiwani Pemba, elimu watakayopatiwa kuitumia vizuri tena kwa vitendo kwa
kuweka mikakati ya kuandika makala mbali mbali, hasa za vijijini kwa vile
waandishi wengi hawafiki huko.
Akisoma risala ya klabu ya waandishi wa habari Pemba
(PPC)katibu wa PPC Khatib Juma Mjaja, alisema PPC imekuwa ikitekeleza shuhuli
mbali mbali za kuwajengea uwezo wanachama wake kwa kuwapatia mafunzo kutoka kwa
wadau mbali mbali.
Alizitaja miongoni mwa shuhuli za kijamii ambazo zimefanywa
ni pamoja na kuendesha na kusimamia miradi ya Ukimwi, madawa ya Kulevya, Afya
ya mama na mtoto, Mazingira na miradi mengine mingi.
“Katika kutekeleza Shuhuli zetu tumekuwa hatusimami pekeyetu
, lakini tumekuwa tukishirikiana na wadau mbali mbali wa habari ikiwemo UTPC,
MCT.
Naye msaidizi katibu wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba,
Ali Mbarouk Omar alisema mafunzo hayao yatazidisha uweledi na uwelewa kwa
waandishi wa habari katika utekelezaji wa kazi zao.
Alilishukuru jeshi la Polisi kwa kuwa mstari wa mbele
kushirikiana na waandishi wa Pemba, kwa kuwapatia habari mbali mbali pale
wanapozihitaji, pamoja na kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Akitoa shukurani kwa niaba ya waandishi wenzake, mwandishi
wa habari mkongwe kisiwani Pemba Ali Khatib Chwaya, waliahidi kufanyia kazi
maagizo yote ya Kamanda kwa kuzingatia taaluma yao.
Aliwataka waandishi wenzake kuhakikisha wanaandika makala
mbali mbali za uchunguzi ili kwenda sambamba na mafunzo hayo wanayopatia.
No comments:
Post a Comment