tangazo

tangazo

Wednesday, December 23, 2015

MKUTANO MKUU WA DHARURA ZFA WAINGIA KIDUDU.



Na: Abubakar Khatib (Kisandu), Zanzibar.
Baada ya jana Jumannne kutangazwa tarehe ya kufanyika mkutano mkuu wa dharura wa ZFA hatimae leo yameibuka mengine mapya.
Makamo wa Urais Unguja wa chama cha mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir “Mpakia” ameibuka na mapya kwa kusema mkutano mkuu hautokuwepo siku ya Jumapili ya tarehe 27 Disemba na utatangazwa tarehe nyengine mpya ya mkutano huo.
Aliyasema hayo wakati alipozungumza na waandishi wa Habari kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Migombani Zanzibar.
“ Mkutano tarehe 27 Disemba hautokuwepo kwasababu sisi viongozi wengine wa juu wa kamati tendaji hatujui, na ZFA haina pesa ya kuendesha mkutano mkuu, pesa tutazipata wapi?, kwaiyo mkutano huo haupo mimi kama makamo wa Urais Unguja ZFA Haji Ameir nasema mkutano haupo”. Alisema Mpakia.
Katika barua ya kuahirishwa mkutano mkuu wa dharura wa ZFA yenye kumbukumbu namba Ref.ZFA/MMM/VOL.1/214 barua ambayo imeandikwa tarehe 22/12/2015 ambapo imesainiwa na wajumbe 8 wakiwemo Haji Ameir, Abdulghan Msoma, Massoud Attai, Ali Bakar, Ahmada Haji, Hashim Salum, Khatma Mwalim na Hussein Ali.
Lakini cha kushangaza Afisa Habari wa ZFA Ali Bakar ambae jana ndio alietoa taarifa ya kuwepo mkutano huo, yumo katika wajumbe 8 waliosaini kutokuwepo kwa mkutano huo, mtandao huu ukamtafuta tena Afisa Habari huyo na kutaka kujua vipi mbona wanawachanganya wadau wa soka , mara mkutano upo, mara haupo, Afisa Habari huyo alizidi kusisitiza kuwa mkutano upo licha ya kuwa na yeye yumo kwenye wajumbe 8 waliotia saini kwa kukataa mkutano kutokuwepo.
“ Mkutano upo siku ile ile ya jumapili ya Disemba 27 na pale pale Aman Judo tutafanya, mimi kweli nimetia saini ya kukataa kutokuwepo mkutano huo, lakini ni shindikizo tu la kutakiwa nisaini , lakini mimi kwenye kikao hicho sijakuwepo nililazimishwa tu, kama afisa habari wa ZFA nasema mkutano upo kama kawaida mpaka anipe taarifa Rais wangu kuwa mkutano haupo. Alisema afisa habari wa ZFA Ali Bakar Cheupe.
Jana afisa habari wa ZFA alitoa taarifa za kuthibitisha kuwepo mkutano huo huku akisema maamuzi hayo yamefikiwa baada ya rais wa chama hicho Ravia Idarous Faina kupata baraka za kamati tendaji za ZFA juu ya kufanyika mkutano huo.
Ajenda kuu kwenye mkutano huo kama ilivyokubaliwa ndani ya kikao cha pamoja kilichosimamiwa rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi ni kuunda kwa kamati maalum ya kushughulikia katiba ya ZFA, Kupitia mahesabu ya ZFA na kuangalia utendaji wa kamati tendaji ya chama hicho.
Shirikisho la soka Tanzania TFF lililazimika kuingilia kati mtafaruku wa soka visiwani Zanzibar baada ya barua kutoka Shirikisho la soka barani Afrika CAF kutishia kuifungia Zanzibar.

No comments:

Post a Comment