WILAYA YA KISARAWE.
Chama cha wananchi cuf kimesema
kuwa iwapo kitapewa mamlaka ya kuongoza dola, kitahakikisha kuwa kinaunda
serikali ya Umoja wa Kitaifa Tanzania, ili kutoa fursa kwa wataalamu wa Itikadi
tofauti za vyama vya siasa kushiriki katika serikali na kuwa kichocheo cha
maendeleo.
Akizungumza na wananchi hao katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Msanga sokoni Wilaya ya
Kisarawe,mkoaniwa pwani katibu mkuu wa chama cha wananchi cuf Maalim Seif
Sharif Hamad amesema kuwa mabadiliko ya kiuongozi yanahitajika katika
kuwakomboa wananchi kiuchumi na kijamii.
amewashauri wanatanzania kuachana na vyama vilivyopoteza muelekeo, na
badala yake kukiunga mkono chama chenye dira ya kuwaletea maendeleo.
Amesema hatma ya maendeleo ya
wananchi iko kwa wananchi wenyewe, na kwamba ndio wenye maamuzi ya kuchagua
uongozi wanaoutaka kwa maendeleo yao na taifa kwa jumla.
Amesema ni jambo la kushangaza
kuona Tanzania imeachwa nyuma kimaendeleo katika kipindi cha miaka 53 ya uhuru,
huku nchi nyengine zilizokuwa hadhi sawa na Tanzania zikipiga hatua kubwa za
maendeleo.
Amezitolea mfano baadhi ya nchi
zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo kuwa ni pamoja Singapore na Malaysia, nchi
ambazo zilikuwa maskini kuliko Tanzania, na kwamba Tanzania ina mengi ya
kujifunzo kutoka nchi hizo.
“Singapore na Malaysia zilikuwa
nchi maskini kuliko nchi yetu, lakini sasa zamepaa hadi dunia ya pili kuelekea
ya kwanza kwa maendeleo. Hii imetokana na uongozi na mipango bora ya maendeleo
waliyojiwekea”, alifafanua Maalim Seif.
Amefahamisha kuwa kitu cha
kushangaza ni kuona Tanzania ina rasilimali nyingi zaidi kuliko nchi hizo
lakini imedumaa kimaendeleo, jambo ambalo linapaswa Watanzania walitafakari kwa
kina na kulitafutia ufumbuzi muafaka.
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar amewaeleza wananchi kuhusu mafanikio yaliyopatikana
Zanzibar tokea kuanzishwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Amesema kuwa kuundwa kwa serikali
hiyo kumetokana na maamuzi ya wananchi wengi wa Zanzibar, na kuwabeza wale
wanaoubeza mfumo huo ambao pamoja na mambo mengine umerejesha amani, umoja na
mshikamano miongoni mwa Wazanzibari.
Ameyataja mafanikio mengine ya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa ni pamoja na kuongezwa kwa bei ya karafuu
kutoka shilingi elfu tatu hadi elfu 15 kwa kilo moja, na kupunguzwa kwa
gharama za pembejeo za kilimo.
Mapema akizungumza katika mkutano
huo, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa CUF Abdul
Kambaya amesema kuwa bado Wilaya ya Kisarawe inakabiliwa na matatizo ya
miundombinu ya barabara, elimu na afya.
Amewasisitiza wananchi wa Wilaya ya kisarawe kubadilisha
mfumo wa uongozi, ili kuwezesha rasilimali za nchi ziweze kutumika vizuri kwa
maslahi ya wananchi wote.
Kabla ya mkutano huo Maalim Seif
alifanya ziara ya kichama katika Wilaya hiyo na kufungua matawi ya CUF, pamoja
na kukabidhi baiskeli ya matairi matatu kwa ndugu Khamis Salum mwenye ulemavu,
ili iweze kumsaidia katika harakati zake za kimaisha.
No comments:
Post a Comment