RAIS WA
ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI DK. ALI MOHAMED SHEIN AMESEMA
TANGU MAPINDUZI YA TAREHE 12 JANUARI, 1964 ZANZIBAR IMEKUWA IKIONGOZWA NA
SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR AMBAYO INA MAMLAKA KAMILI YANAYOHESHIMIWA
NDANI NA NJE YA JAMHURI YA MUNGANO WA TANZANIA.
AMEFAFANUA
KUWA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR NI SERIKALI HALALI INAYOTAMBULIWA KOTE
ULIMWENGUNI HUKU IKIWA INAONGOZWA CHINI YA MIHIMILI MIKUU MITATU; KATIBA,
BARAZA LA KUTUNGA SHERIA NA MAHKAMA ILIYO HURU.
DK. SHEIN
AMBAYE PIA NI MAKAMU MWENYEKITI WA CCM ZANZIBAR ALISEMA HAYO JANA WAKATI
ALIPOKUWA AKIZUNGUMZA NA MAELFU YA WANANCHI WALIOHUDHURIA UZINDUZI WA
MAADHIMISHO YA MIAKA 37 YA KUZALIWA CHAMA CHA MAPINDUZI ULIOFANYIKA KATIKA KIWANJA
CHA MICHEZO CHA KIEMBESAMAKI, WILAYA YA MAGHARIBI, MKOA WA MJINI MAGHARIBI
UNGUJA.
“ZANZIBAR
INA BENDERA YAKE, INA RAIS WAKE NA HIVYO HAKUNA ANAYEWEZA KUINGILIA MAMLAKA YA
ZANZIBAR” ALISISITIZA DK. SHEIN HUKU AKIULIZA HAO WANAODAI ZANZIBAR ILIYO NA
‘MAMLAKA KAMILI’ WANATAKA NINI HASA.
ALISISITIZA
KUWA HAKUNA ANAYEINGILIA MASUALA YA ZANZIBAR NA KUELEZA KUWA ZANZIBAR
INAENDESHWA KWA MUJIBU WA KATIBA YAKE AMBAYO INAHESHIMIWA KAMA INAVYOHESHIMIWA
KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
“SERIKALI YA
MAPINDUZI INAJIAMINI NA INAENDESHWA KWA MUJIBU WA KATIBA YAKE AMBAYO
INAHESHIMIWA NA KATIBA YA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, SASA NANI
ANAYEISHUSHIA HADHI SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR?”DK. SHEIN ALIHOJI.
ALIWASHANGAA
WATU WANAODAI KUTAKA ZANZIBAR YENYE ‘MAMLAKA KAMILI’ NA KUWAULIZA MAMLAKA HAYO
KUTOKA WAPI WAKATI ZANZIBAR TANGU MAPINDUZI YA MWAKA 1964 IMEKUWA IKIJIENDESHA
YENYEWE NA KUFANYA MAMBO YAKE BILA KUINGILIWA NA MTU.
DK. SHEIN
ALIREJEA MSIMAMO WA CHAMA CHA MAPINDUZI KUHUSU MABADILIKO YA KATIBA NA KUSISITIZA
KUWA CHAMA HICHO KINASIMAMIA SERA YAKE YA MUUNGANO WA SERIKALI MBILI.
“KILA MTU
AMETOA MAONI YAKE KUHUSU KATIBA NA SISI TUNAONGOZWA NA SERA YETU, KATIBA YETU
NA ILANI YETU HIVYO KATIKA HILI LA MUUNGANO SISI TUMESIMAMA KWENYE MUUNGANO WA
SERIKALI MBILI” DK. SHEIN ALIELEZA HUKU AKISHANGILIWA NA WANA CCM NA WANANCHI
WALIOHUDHURIA MKUTANO HUO.
ALISISITIZA
KUWA CHAMA CHA MAPINDUZI HAKITARUDI NYUMA KATIKA MSIMAMO WAKE HUO NA KUSISITIZA
KUUENZI KUULINDA NA KUUENDELEZA MUUGANO HUO.
ALIWAELEZA
MAELFU YA WANANCHI WALIOKUWA WAKIKATISHA HOTUBA YAKE MARA KWA MARA KWA NDEREMO
KUWA WANA CCM NA WANANCHI WANAPOADHIMISHA MIAKA 37 YA KUZALIWA KWA CCM NI
KUDHIHIRISHA KUMBUKUMBU YA USHINDI WA VYAMA VYA AFRO SHIRAZI NA TANU
VILIVYOWASHINDA WAKOLONI NA KUWALETEA WANANCHI UHURU WAO.
“TUNAPOADHIMISHA
MIAKA 37 YA CCM AMBACHO NI MATOKEO YA MUUNGANO WA HIARI WA VYAMA VYA ASP NA
TANU, TUNAADHIMISHA PIA KUMBUKUMBU YA USHINDI WA VYAMA VYETU HIVYO DHIDI YA
WAKOLONI NA KUTULETEA UHURU WETU” DK. SHEIN ALISEMA.
ALIFAFANUA
KUWA WAASISI WA VYAMA HIVYO WAKIONGOZWA NA MZEE ABEID AMANI KARUME NA MWALIMU
JULIUS NYERERE WALIFANYAKAZI KUBWA YA KUWAONDOA WAKOLONI NCHINI AMBAPO KWA
UPANDE WA ZANZIBAR ILIBIDI WAFANYE MAPINDUZI KULETA UHURU BAADA YA NIJA ZA
KAWAIDA KUSHINDIKANA.
ALIWAKUMBUSHA
WANA CCM NA WANANCHI KWA JUMLA KUWA MIEZI MICHACHE IJAYO WATAADHIMISHA MIAKA 50
YA MUUNGANO KATI YA JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR NA JAMHURI YA TANGANYIKA
ULIOZAA JAMHURI YA MUUGANO WA TANZANIA HIVYO NI WAKATI MUAFAKA KWAO KUZINGATIA
KUMBUKUMBU HIYO MUHIMU KATIKA HISTORIA YA KUJITAWALA.
MAKAMU
MWENYEKITI HUYO WA CCM ALITUMIA FURSA HIYO KUMTAMBULISHA MGOMBEA NAFASI YA
UWAKILISHI KATIKA UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA KIEMBESAMAKI MAHMOUD THABIT KOMBO
NA KUWATAKA WANANCHI KUMPIGIA KURA ILI CCM IWEZE KUKAMILISHA UTEKELEZAJI WA ILANI
YAKE KATIKA JIMBO HILO.
AKIZUNGUMZA
KATIKA MKUTANO HUO KATIBU MKUU WA CCM KANALI MSTAAFU ABDULRAHMAN KINANA
ALIMPONGEZA MAKAMU MWENYEKITI WA CCM ZANZIBAR KWA KUKIONGOZA CHAMA HICHO KWA
UMAHIRI MKUBWA NA KUIFANYA ZANZIBAR KUENDELEA KUWA TULIVU NA YENYE UMOJA.
AMESEMA CCM
ILIZALIWA ZANZIBAR MIAKA 37 ILIYOPITA KISIWANI UNGUJA NA HADI LEO SERIKALI ZOTE
MBILI ZIMEENDELEA KUONGOZWA NA CHAMA HICHO HIVYO NI USHINDI MKUBWA KWA WANA
CCM.
KATIBU MKUU
HUYO ALIWAPONGEZA WANANCHI WA ZANZIBAR KWA KUADHIMISHA MIAKA 50 YA MAPINDUZI NA
KUWATAKA KUJIVUNIA MAENDELEO WALIYOYAPATA KATIKA KIPINDI HICHO CHA MIAKA 50.
“MAADHIMISHO
HAYO NI USHINDI MKUBWA KWA WANANCHI WA ZANZIBAR KWA KUWA NDANI YA MIAKA 50 HIYO
WAKO WALIYOYABEZA NA WAKO WALIOJITAHIDI KUYAPINGA KWA NGUVU ZAO ZOTE LAKINI
WAMESHINDWA NA LEO HII YAMEFIKIA MIAKA 50 NA YATADUMU NA 50 MINGINE”
ALISISITIZA KINANA.
ALIWAELEZA
WANANCHI HAO KUWA CHAMA CHA MAPINDUZI KITAENDELEA NA JUKUMU LAKE LA KUWALETEA
MAENDELEO WANANCHI KWA KUTEKELEZA MIPANGO MBALIMBALI YA MAENDELEO KAMA ILIVYOELEZWA
KATIKA ILANI YAKE YA UCHAGUZI PAMOJA NA MIPANGO YA KITAIFA.
ALIWAAMBIA
WANA CCM HAO KWAMBA CHAMA CHA MAPINDUZI DAIMA KITAENDELEA KUTEKELEZA JUKUMU
LAKE LA KUTENDA MEMA KWA WANANCHI WOTE WA TANZANIA WAKATI VYAMA VYA UPINZANI
VITAENDELEA NA JUKUMU LAO LA KUSEMA. “KUSEMA RAHISI KULIKO KUTENDA” ALISEMA
KATIBU MKUU WA CCM.
UZINDUZI WA
SHEREHE HIZO ULIHUDHURIWA NA VIONGOZI MBALIMBALI WA CCM AKIWEMO MJUMBE WA
KAMATI KUU AMBAYE PIA NI MAKAMU WA PILI WA RAIS BALOZI SEIF ALI IDDI NA NAIBU
KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR BWANA VUAI ALI VUAI.
No comments:
Post a Comment