ZANZIBAR.
Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imesema iko tayari kushirikiana na Serikali ya Italia katika nyanja za
elimu na hifadhi ya sehemu za historia kama ilivyo katika sekta nyingine.
Hayo yameelezwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati
akizungumza na Balozi wa Italia nchini Bwana Luigi Scotto aliyemtembelea Ikulu
MJINI ZABNZIBAR.
Katika mazungumzo hayo Balozi
Luigi alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imeanzisha Mpango wa Ushirikiano Kati
ya Italia na Afrika ambao umelenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hiyo na
nchi za Afrika.
Alibainisha kuwa chini ya mpango
huo Zanzibar inaweza kufaidika katika suala la uhifadhi na ukarabati wa sehemu
za historia kama vile Mji Mkongwe pamoja na masuala ya ufundishaji wa lugha ya
Kitaliano hapa nchini.
Dk. Shein alimueleza Balozi
Luigi kuwa ukarabati na uhifadhi wa mji Mkongwe ni suala linalopewa umuhimu
mkubwa na Serikali hivyo fursa ya kushirikiana na Serikali ya Italia katika
suala hilo imekuja wakati muafaka.
Aliongeza kuwa mpango wa
kufundisha ya lugha ya kitaliano nao ni muhimu na unaweza kutekelezwa kupitia
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar-SUZA chini ya Skuli ya Kiswahili na Lugha za
Kigeni katika chuo hicho.
Dk. Shein alimhakikishia Balozi
Luigi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufanyakazi na Serikali
ya Italia ili kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi mbili hizo.
NAYE Balozi Luigi Scotto
kwa upande wake alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake inaupa umuhimu mkubwa
uhusiano wake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Zanzibar ikiwemo.
Alifafanua kuwa mbali ya
uwekezaji mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanywa na wananchi wa Italia humu
nchini, nchi mbili hizo zina mambo yanayofanana kama vile sehemu nyingi za
kihistoria.
No comments:
Post a Comment