Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi
CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema wakati umefika kwa viongozi wa
Afrika kufuata maoni na matakwa ya wananchi, ili kuepusha migogoro isiyo ya
lazima baina ya viongozi na wananchi.
Amesema mara nyingi wananchi
huamua kupingana na serikali baada ya kuona haki zao za msingi zinakiukwa,
jambo ambalo serikali za sasa zinapaswa kuzingatia madai na haki za wananchi
ili kuondosha mivutano hiyo.
Mhe. Maalim Seif ametoa nasaha
hizo wakati akizungumza kwenye mkutano wa tisa wa Muungano wa vyama vya
Kiliberali na Democrat kwa baadhi ya nchi za Ulaya, Pacific, Afrika na
Caribbean (ALDEPAC), unaofanyika mjini Cape town nchini Afrika ya
Kusini.
Amesema wananchi wamekuwa
wakikabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ambayo
wanapoyapeleka serikalini huwa hayazingatiwi, hali inayopelekea kuibua hamasa
miongoni mwa wananchi kuanzisha makundi haramu kupingana na serikali.
Mhe. Maalim Seif ambaye ni Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema iwapo madai ya wananchi yatasikilizwa na
kupatiwa haki zao za msingi hasa zile za kikatiba, pamoja kuzingatiwa kwa
tatizo la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, mivutano baina ya wananchi na
serikali zao inaweza kupungua.
Ametaja matatizo yanayozisumbua
nchi nyingi za Afrika kuwa ni pamoja na umasikini, njaa, ukosefu wa ajira na
utawala bora.
Amewaambia wajumbe wa mkutano huo
kwamba Afrika sio tena bara lenye kiza, bali raia wake wameamka na kudai mabadiliko
ya kiuchumi na kisiasa ili kila raia aweze kuishi katika maisha bora yenye
tija.
“Waafrika sasa wanahitaji
maendeleo ya kiuchumi, elimu bora, huduma za afya, maji safi na salama pamoja
na kuungwa mkono katika miradi yao ya maendeleo”, alifahamisha Maalim Seif na
kuongeza,
“Kubwa zaidi wananchi wanataka
uwajibikaji na uwazi katika serikali zao, pamoja na kuwepo uhuru wa kutoa maoni
na kuheshimiwa kwa haki za binadamu”.
Amemshukuru Rais wa Muungano wa
vyama vya Kiliberali Barani Afrika, Olivier Kamitatu, kwa kuamua kufanya
mkutano wao mkuu Zanzibar mwezi uliopita, ambao amesema ulikuwa na mafanikio
makubwa.
Mhe. Maalim Seif yuko nchini Afrika ya Kusini
kwa mwaliko maalum wa muungano wa vyama vya kiliberali kuhudhuria mkutano huo.
No comments:
Post a Comment