ZANZIBAR.
Jeshi la Polisi nchini limesema KUWA litaendelea
kushirikiana na raia katika jitihada zake za kukabiliana na vitendo vya
uhalifu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Jeshi la
Polisi nchini IGP Ernest Mangu, wakati akizungumza na MakamO wa KWanza wa Rais
wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,
ofisini kwake Migombani.
IGP Mangu
ambaye alikuwa amefuatana na Naibu wake Abrahmani Kaniki pamoja na kamishna wa
polisi Zanzibar Hamdani Omar Makame, amesema suala la kudhibiti uhalifu ndio
jukumu la msingi la jeshi la polisi, na kwamba litafanya kila juhudi kuona kuwa
vitendo vya uhalifu vinadhibitiwa.
Ameongeza kuwa jeshi la polisi kamwe halipendi
kuona kuwa linakuwa chanzo cha vurugu, bali kuzuia vurugu pale zinapotokea na
kurejesha amani pale inapotoweka.
Aidha IGP Mangu amesema jeshi hilo litaendelea
kushirikiana na serikali katika jitihada zake za kukuza uchumi na kupunguza
umaskini, kwa kutunza usalama katika maeneo ya utalii ambao ndio sekta kiongozi
kwa uchumi wa Zanzibar.
Amefahamisha kuwa suala la amani na usalama ni
jambo la msingi katika nchi, na kwamba hali hiyo ndio msingi mkuu wa kuvutia
wawekezaji wa sekta mbali mbali hasa utalii.
Hivyo amesema wataweka mkazo katika maeneo ya
utalii ili kuhakikisha kuwa hakuna vitisho wala madhara yanayopatikana kwa
wageni wanaoingia nchini.
IGP Mangu amesema ingawa jeshi hilo bado
linakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi vya kisasa, lakini watatumia
rasilimali zilizopo katika kuimarisha utendaji wake.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.
Maalim Seif Sharif Hamad amesema suala la ulinzi wa raia na mali zao linapaswa
kupewa kipaumbele cha mwanzo katika utendaji wa jeshi hilo.
Amesema amani na usalama ndio chachu ya
maendeleo kwa uchumi wa Zanzibar ambayo inategemea zaidi sekta ya utalii.
Amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi aliyepita
IGP mstaafu Said Mwema, kwa wazo lake la kuanzisha polisi jamii ambayo imeliweka
karibu zaidi jeshi hilo na wananchi.
Amemtaka IGP Mangu kuliendeleza wazo hilo,
kwani linasaidia kuondosha khofu kwa raia dhidi ya polisi.
Amesisitiza haja kwa jeshi la polisi kuendeleza
mahusiano mema na raia, ili kuwawezesha wananchi kujenga imani na jeshi hilo,
hatua ambayo itasaidia utendaji wa jeshi.
NAYE
MakamO wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amemTAKA IGP Mangu ya kulisafisha jeshi hilo dhidi ya
vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kuliandama jeshi hilo.
Amesema katika kulisafisha jeshi hilo dhidi ya
vitendo vya rushwa, hakuna budi kwa viongozi kuondosha muhali wakati wanapoamua
kuwashughulikia watendaji wanaoendesha vitendo hivyo.
No comments:
Post a Comment