Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amefanya mabadiliko katika baraza lake la
mawaziri kwa kuwateua mawaziri na manaibu waziri, kuziba nafasi zilizoachwa na
mawaziri wanne waliojiuzulu na mmoja aliyefariki dunia hivi karibuni.
Katika uteuzi huo
Rais Kikwete amewateua mawaziri wapya wawili na manaibu waziri wapya wanane,
huku akiwapandisha vyeo manaibu waziri wanne kuwa mawaziri kamili.
Miongoni mwa
mawaziri wapya ni pamoja na aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Dokta Asha-rose Migiro, ambaye ameteuliwa kuwa waziri wa Katiba na
Sheria, huku Dk. Titus Kamani akiteuliwa kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi.
Waziri pekee
aliyeachwa katika mabadiliko hayo ni aliyekuwa waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Rais, (Mazingira), Dk. Terezya Huvisa.
Miongoni mwa
manaibu waziri wapya ni pamoja na Juma Nkamia ambaye kitaaluma ni mwandishi wa
habari na mtangazaji, ambaye amepewa dhamana katika Wizara ya Habari, Vijana na
Michezo.
Mabadiliko
yaliyofanywa na Rais Kikwete yametokana na kujaza nafasi za mawaziri ambao
walilazimika kujiuzulu baada ya ripoti ya bunge kuhusu Operesheni Tokomeza
Ujangili kubaini kuwepo vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwa ni
pamoja na mauaji, utesaji na udhalilishaji vikidaiwa kutendwa na watekelezaji
wa operesheni hiyo.
Ripoti hiyo
iliwalazimisha waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kutangaza
kujiuzulu, huku naye waziri wa mambo ya ndani, Dr. Emmanuel Nchimbi kufuata
mkondo huo bila kumwaacha waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa, Shamsi
Vuai Nahodha, na Dr.
Mathayo David
Mathayo aliyekuwa waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kutokana na wizara
zao kuhusika katika usimamizi wa operesheni hiyo ambayo iliwahusisha polisi,
askari jeshi na walizni wa wanyamapori.
Huku nafasi ya
tano katika baraza hilo ikiachwa wazi na aliyekuwa waziri wa fedha, Dr. William
Mgimwa aliyefariki dunia mapema mwezi huu nchini Afrika Kusini alikokuwa
akipata matibabu.
No comments:
Post a Comment