tangazo

tangazo

Monday, January 12, 2015

Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wauguzi kuacha kufanya kazi kwa mazoea

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wauguzi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike kifikra na mawazo katika kutekeleza majukumu yao.
Hayo ameyaeleza katika Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja Wilaya ya Mjini Unguja wakati wa Ufunguzi wa Wodi mpya ya Wagonjwa Mahututi (ICU) ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 51 ya sherehe ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema wauguzi wana dhamana kubwa ya kuokoa maisha ya watu hivyo wanajukumu la kuhakikisha wanatoa huduma iliyo bora na ya uhakika.
Maalim  Seif amesema wauguzi wa wagonjwa mahututi (ICU) wana haki ya kupata mafunzo ili waweze kutoa huduma hiyo kwa ufanisi wa hali ya juu ili kufikia lengo lililokusudiwa.
“Wafanyakazi kuwa wapole, wenye kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa, kuwa wastahamilivu na waliotayari katika kutoa huduma zao”, amesema Maalim Seif.   
Amewataka wafanyakazi wa ICU kuwa wawazi katika kutoa taarifa zinazohusu maendeleo ya wagonjwa pale inapohitajika ili kuondosha usumbufu kwa ndugu na jamaa wanapotaka kupata taarifa hizo.
Aidha amewataka wananchi kufuata taratibu zilizowekwa ili kuepusha usumbufu na matatizo zaidi kwa wagonjwa wa sehemu hiyo.
Maalim Seif amewataka wananchi kutumia vyema huduma hiyo muhimu ili iweze kudumu na kupunguza gharama za usafirishaji wa wagonjwa hao kufuata huduma nje ya nchi.
Mapema Waziri wa Afya Seif Rashid Suleiman amesema huduma ya ICU ni muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu na ni lazima ipate zana za uchunguzi za uhakika ili kuweza kufanya matibabu ya uhakika na usahihi.
Amefahamisha kuwa Wizara imeandaa mpango maalum wa kuratibu dawa zinazotumika nchini kupitia Bohari Kuu ya dawa na Mfamasia mkuu wa serikali kuwacha kuagiza dawa zisizotumika ili kupunguza gharama na hasara.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Mohamed Saleh Jidawi amesema Wodi ya ICU ina vifaa vya kutosha na huduma zote zinapatikana bila ya usumbufu katika wodi hiyo.
Wodi hiyo imegharimu zaidi ya Dola millioni moja hadi kukamilika kwake ambayo ina vitanda nane na inajitosheleza kwa huduma zote zinazohitajika kwa wagonjwa.

No comments:

Post a Comment