ZANZIBAR.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Idara Maalum za SEREKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR Haji Omar Kheri amewataka
wafanyakazi wa Shirika la Bandari Zanzibar kufanya kazi kwa juhudi na ufanisi
kwa lengo la kuleta maendeleo na mabadiliko nchini.
WAZIRI HUYO AMEELEZA HAYO katika Shirika la Bandari Zanzibar wakati
akizindua Tagi mpya ya Shirika hilo MV Shuwari ikiwa ni miongoni mwa
shamrashamra za kusherehekea miaka 51 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema KUWA bandari ni chachu ya maendeleo katika
nchi yoyote Duniani na muhimili mkuu wa kuleta maendeleo na mabadiliko
yatakayofanywa kwa ufanisi na juhudi kubwa zitakazoweza kuinua uchumi wa
nchi.
Amefahamisha kuwa utendaji wa kazi unategemea
rasilimali watu na vifaa vya kisasa vinavyo kwenda sambamba na mazingira ya
kazi yatakayoleta maendeleo na mabadiliko ya haraka katika kutoa huduma za
utendaji.
Aidha Waziri Omar ameeleza kuwa ufinyu wa
nafasi ya kuhifadhia mizigo bandarini hapo, pamoja na Wafanyabiashara
kutoondosha Makontena yao kwa wakati ndio changamoto kubwa zinazoikabili
bandari hiyo.
Waziri Omar pia amewataka wafanyabiashara
kuchukua juhudi za kutoa mizigo yao bandarini kwa wakati ili kuondosha
msongamano uliopo na kulipa ushuru wa mizigo hiyo ili kuliongezea pato la
Taifa.
Amesema madhumuni ya Tag hiyo ni kuimarisha
ufungaji na ufunguaji wa meli bandarini hapo hivyo mategemeo makubwa ni kuona
kuwa inatumika ipasavyo kwa kufuata ushauri na maelekezo ya wataalamu kwa lengo
la kuleta maendeleo ya bandari na taifa kwa ujumla.
Nae Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Bandari
Zanzibar CAPTEN Abdalla Juma Abdalla amesema KUWA Tagi Mv Shuwari tayari
imeshaanza kazi ya kusaidia kufunga na kufungua meli gatini ambayo inauwezo wa
kukabiliana na majanga ya moto pamoja kusaidia kuokoa maisha ya watu inapotokea
ajali ya meli au boti baharini.
Amesema Tagi hiyo imejengwa kwa udhamini wa
kampuni ya Damen Shipyards ya Uholanzi kwa kushirikiana na Shirika la Bandari
la Zanzibar na imegharimu Tsh.zaidi Bilioni 10 ambapo Bilioni 6.9 ni mkopo
kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na ghrama zilizobaki zimelipwa na
Shirika la Bandari.
No comments:
Post a Comment