ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa mwaliko wa Zanzibar kushiriki katika Tamasha la Kimataifa la
Muziki wa Afrika nchini Ujerumani mwezi Juni mwaka huu, ni njia moja wapo ya
kuitangaza Zanzibar kiutalii nchini humo pamoja na nchi nyengine za Ulaya.
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika mazungumzo kati yake na Balozi wa
Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Egon Kochanke aliyefuatana na Dk. Stefan Oscman
ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Tamasha la Afrika, mazungumzo
yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alisema kuwa mwaliko huo ni nafasi ya
pekee kwa Zanzibar kuweza kujitangaza kiutalii pamoja na kiutamaduni, kutokana
na Zanzibar kujaaliwa katika sekta hizo ambazo zimeweza kuijingea sifa kubwa
ndani na nje ya nchi.
Dk. Shein alisema kuwa Ujerumani na Zanzibar ni nchi zenye uhusiano wa
kihistoria ambao umeweza kuleta mashirikiano makubwa katika sekta mbali mbali,
na kusisitiza kuwa hatua hiyo ni ya pekee kwa Zanzibar, ambayo itaweza kusaidia
katika mikakati yake ya kukuza uchumi na kuimarisha utamaduni.
Aidha, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Ujerumani kwa kuithamini
Zanzibar. na kuipa mwaliko katika tamasha hilo, sambamba na kushiriki
kikamilifu kwa wasanii wa Zanzibar ambao wataonesha tamaduni za kizanzibari.
No comments:
Post a Comment