tangazo

tangazo

Thursday, January 8, 2015

SERIKALI INAANDAA ZOEZI LA UTAMBUZI WA WAZEE WA KUANZIA MIAKA 60



ZANZIBAR.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na watoto IMESEMA KUWA inaandaa zoezi la utambuzi wa wazee wenye umri  kuanzia miaka 60 na kuendelea ili kuFAHAMU  sehemu wanazoishi na kuwaandalia mazingira mazuri ya maisha yao.
 Akizungumza katika mkutano wa Kamati Tendaji ya Mpango huo katika Wizara ya Uwezeshaji Mwanakwerekwe, Mkuu wa kitengo cha Hifadhi ya Jamii Zanzibar Salum Rashid amesema zoezi hilo litafanywa  katika shehia zote za Zanzibar.
Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba baada ya wazee hao kutambuliwa watapewa kadi maalum ambazo zitawasaidia kwenye huduma muhimu za msingi za kijamii zinazotolewa na Serikali  zikiwemo usafiri na matibabu bila malipo.
Salum amesema maandalizi ya zoezi hilo yako katika hatua nzuri na litafanywa kwa uangalifu mkubwa ili  kuhakikisha kila aliefikia umri huo aweze kuoredheshwa kupitia shehia wanazoishi.
Katika kufanikisha mpango huo Wizara itaandaa vijana  wasiopungua 45 na kuwapa mafunzo  ya kazi hiyo  na  kila shehia itakuwa na kijana mmoja ambae atashirikiana na  sheha ama mjumbe wake.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Zanzibar inaowazee 58311 wenye umri wa  kuanzia miaka 60  ambao ni sawa na asilimia 4.5 ya wananchi wote.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na  Shirika la HelpAge mwaka 2009, asilimia 60 ya  wazee wenye umri huo hawana kipato rasmi cha kuendeleza maisha yao  na baadhi yao wamekuwa wakipata msaada mdogo kutoka kwa jamaa zao.
Amesema kutokana na usumbufu wa maisha unaowapata wazee hao ndipo Serikali ikaamua kuandaa mpango huo ili waweze kupatiwa msaada.
Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Msham Abdalla Khamis amesema  zoezi hilo halina uhusiano wowote na masuala ya siasa hivyo amewataka wananchi wasiwe na wasi wasi .
HATA  HIVYO  KIONGOZI HUYO amesema lengo kuu la  mpango huo ni kuwatambua wazee sehemu wanazoishi  ili kuwasaidia  waweze kujikimu kimaisha na kuwapatia baadhi ya huduma muhimu za kijamii bila malipo.

No comments:

Post a Comment