Wilaya ya kaskazini b.
Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi
amesema kuwa jukumu la Wazazi na
Walezi Nchini bado litaendelea kubakia pale pale katika kuhakikisha
kwamba wanasimamia vyema watoto wao kupata Elimu kadri ya uwezo wa watoto hao
utakavyowaruhusu.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar alieleza hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vifaa mbali mbali
vya ujenzi kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo jipya la Skuli ya Msingi ya
Kinduni iliyomo ndani ya Jimbo la Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema kuwa tabia ya kuwaharakisha watoto wao
katika maisha yao hasusan wa kike kuwaozesha mapema wakufahamu kwamba
wanawadumaza katika kupata wataalamu na viongozi bora wa hapo baadaye.
Vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na
Matofali, Nondo, Saruji, Mchanga na Kokoto vitasaidia nguvu za Wananchi wa
Kijiji cha Kinduni walioamua kukabiliana na ufinyu na nafasi za Madarasa kwa
watoto wa Kijiji hicho na vile vya jirani.
Balozi Seif alisema kundi kubwa la watoto kwa
kushirikiana na wazazi wao walioamua kutafuta elimu kwa njia zote ndilo
litakalofanikiwa kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya Teknolojia katika
karne ijayo.
Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope amewapongeza
Walimu wa Skuli ya Kinduni kwa juhudi wanazochukuwa katika kuwapatia
elimu wanafunzi wao na kufanikiwa kupasisha wanafunzi wengi waliyoipatia sifa
skuli hiyo kushika nafasi ya Tatu Kitaifa kwa wanafunzi walioingia Mchepuo.
Akitoa Taarifa fupi ya Skuli ya Msingi Kinduni
Mwalimu Mkuu wa Skuli hiyo Bibi Miza Omar Moh’d alisema mchango wa Mbunge wa
Jimbo la Kitope kwa Skuli hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009 unaendelea kuleta
faraja kwa wazazi, walimu na wanafunzi wa skuli hiyo.
Mwalimu Miza alisema licha ya changamoto ya
upungufu wa walimu, ukosefu wa huduma za maji safi na salama, maabara na
Maktaba lakini lengo la Kamati ya Uongozi ya Skuli hiyo ni kuona Kijiji
cha Kinduni kinakuwa na Skuli ya Sekondari.
No comments:
Post a Comment