ZANZIBAR.
Waumini wa Dini ya Kiislamu, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Viongozi wa Serikali Vyama vya siasa pamoja na Wananchi, jana jioni walihudhuria
Hitma ya kumuombea Dua aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni almarhoum
Salmin Awadh Salmin.
Hitma hiyo ilyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa wa Nur Muhammad Mtaa
wa Mombasa kwa Mchina, iliongozwa na Imam wa Msikiti huo Sheikh Othman Maalim
akisaidiwa na Naibu wake Sheikh Jaffar Abdulla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Waziri
Kiongozi Mstaafu Mh. Shamsi Vuai Nahodha, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Vuai Ali Vuai na baadhi ya Mawaziri walijumuika na waumini hao katika hitma
hiyo.
Mwakilishi huyo wa Jimbo la Magomeni alifariki Dunia Alhamisi
ya Tarehe 19/2/2015 baada ya kuugua ghafla akiwa katika Kikao cha kikazi cha
chama hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Marehemu Salmin Awadh Salmin alikuwa pia mnadhimu wa Chama cha
Mapinduzi ndani ya Baraza la Wawakilishi, ambapo kwa wadhifa huo umempa
fursa ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha
Mapinduzi.
Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa
Baraza hilo Jimbo la Kikwajuni Mh. Mahmoud Mohammed Muussa, kwa niaba ya
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Familia ya Marehemu Salmin Awadh
amewashukuru watu wote waliochangia kufanikisha mazishi ya Kiongozi huyo.
Marehemu Salim Awadh Salmin aliyezaliwa Tarehe 6 June Mwaka 1958 na
kuzikwa Kijiji kwao Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja ameacha Kizuka na watoto
wanane.
Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi amin.
No comments:
Post a Comment