Zanzibar.
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amesema kuwa
ziara ya Rais wa Shirikisho la Jamhuri
ya Ujerumani nchini Joachim Gauck ni
fursa nyengine muhimu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya
Zanzibar na Ujerumani.
Akizungumza na Rais huyo Ikulu mjini zanzibar Dk.
Shein amesema kuwa historia inaonesha kuwa uhusiano kati ya Zanzibar na
Ujerumani ulioanza mwaka 1847 ikiwa nchi ya tatu baada ya Marekani na Uingereza
kuanzisha mahusiano na Zanzibar.
aidha dr shein Alitumia fursa hiyo kuishukuru
Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa misaada yake mbali mbali
kuunga mkono jitihada za wananchi za kujiletea maendeleo.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Jamhuri
ya Ujerumani Joachim Gauck alimueleza Dk. Shein kuwa amefurahi kuona Zanzibar
ni nchi yenye kukusanya watu wa tamaduni nyingi pamoja na dini tofauti lakini
wameweza kuishi kwa amani na mashirikiano makubwa.
Rais huyo alieleza kuwa wananchi wa Ujerumani
wanafahamu uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi yao na Zanzibar na kwamba
amekuja hapa kuangalia namna nchi hiyo inavyoweza kuimarisha zaidi uhusiano
huo.
Gauck amesema kuwa watu wa Ujerumani wamekuwa
wakipata taswira nzuri ya Zanzibar kutokana na watalii wanaotembelea Zanzibar
na Tanzania mara kwa mara.
Kuhusu hali ya kisiasa nchini Rais Joachim
Gauck alisema kuwa amefurahi kuona
wananchi wa Tanzania kuwa ni watu
wanaowasiliana na kujadiliana mambo yao bila ya ugomvi na hilo ni jambo kubwa kwa maendeleo ya
demokrasia.
Amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea
kushirikiana na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ili
kuuenzi na kuimarisha uhusiano na ushirikiano huo.
Rais huyo aliwasili leo mchana kwa boti ya
Kilimanjaro 4 inayomilikiwa na Kampuni ya Azam Marine na kupokelewa katika
bandari ya Malindi Zanzibar na viongozi mbali mbali wakiongozwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Rais Joachim alipewa heshima zote kwa kupigiwa
mizinga, na kukagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania –JWTZ.
No comments:
Post a Comment