tangazo

tangazo

Saturday, February 7, 2015

WAZAZI NCHINI WAMETAKIWA KUWA NA UVUMILIVU NA UPENDO NA WATOTO WAO



wilaya ya magharibi.

Walimu, wazazi na walezi nchini wametakiwa kuwa na uvumilivu na upendo kwa watoto wao ili waweze kuwatunza vizuri na kuwapatia elimu bora kwa maisha na maendeleo yao ya baadae,jamii na taifa kwa jumla.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ZAINAB OMAR MOH’D wakati akiwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. 

MSHAM ABDALLA KHAMIS  huko Meli nne, Mwanakwerekwe  wakati wa tafrija na chakula cha mchana alichowaandalia wanafunzi wa chekechea na msingi wa skuli ya KV Academy ili kuwaunga mkono na kuwahamasisha kupenda na kuthamini masomo yao na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema wadau wote hao wana kazi ngumu ya kuwalea na kuwaelimisha watoto ili kuwakomaza kiakili na kuwapatia ujuzi utakaowapelekea  kufanya kazi kwa faida na maendeleo yake, jamii na taifa kwa ujumla.

Mhe Waziri  Zainab amefahamisha kuwa walimu wanajitahidi sana kubadilisha akili za watoto na hatimae kupata vijana wazuri kitabia na wenye uelewa na kusema kuwa ni wajibu wa wazazi na walezi kuwa na mashirikiano ya karibu na kushiriki kuona maendeleo ya watoto wao.

Aidha amewapongeza waanzilishi wa skuli hiyo kwa kuwawekea watoto na jamii rasilimali nzuri ya elimu na kuwaomba wasamaria wema wengine kusaidia maendeleo ya KV Academy ili kuunga mkono na kuiga mfano ulioonyeshwa katika eneo hilo.

Nae Mkurugenzi wa KV Academy Nd. SIMAI MKADAM HAJI ameishukuru Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii,Vijana, Wanawake na Watoto kwa mashirikiano na misaada yake kupitia kwa Mhe. Waziri Zainab ambae ni mlezi wa Skuli hiyo.

Amesema moja ya mafanikio ya skuli hiyo ni pamoja na kuwapatia ajira ya kudumu walimu kumi na tano (15) ambao zaidi ya asilimia 98 ni wanawake ambao awali wakisoma masomo ya ziada skulini hapo na sasa wanfanya kazi ili kukidhi maisha yao.

Akitaja changamoto za Skuli yake,Mkurugenzi huyo wa KV Academy amesema wamekabiliwa na ukosefu wa vifaa vya kufundishia,kuchezea, usafiri na komputa za kufanyia kazi, hivyo amewaomba wahisani wengine kuwasiliana na KV Academy ili kusaidia kuondoa changamoto zilizopo.

No comments:

Post a Comment