MAHAKAMA ya wilaya Makunduchi, imeahirisha tena
kesi ya shambulio la kuumiza mwili, inayomkabili mshitakiwa Ivan Kode
raia wa Ufaransa hadi Februari 12 mwaka huu, ili kupata muda wa kupitia ombi
linalobishaniwa na pande mbili za mahakama.
Mshitakiwa Ivan Kode, anatuhumiwa kuwashambulia kwa
kuwapiga bastola yenye risasi za chubwi, Nadir Ali Juma, Ashraf Suleiman
Yussuf, Wadi Ame Khamis na Ally Ramadhan Mohammed na kuwasababishia maumivu
makali mwilini.
Katika mahakama hiyo iliokuwa chini ya hakimu
Mohammed Ali Haji, Wakili wa mshitakiwa huyo Elizabeth Lazaro Mayalla,
aliiomba mahakama kutoa idhini ya kukabidhiwa paspoti mteja wake ili aweze
kusafiri nje ya nchi kwa matibabu.
Alidai hali ya afya mteja wake ambae hajafika
mahakamani hapo kwa vikao vinne sasa tokea alipotoka mahabusu na kupewa
dhamana, haiko vyema hivyo anahitaji matibabu ya ziada nje ya nchi.
Wakili huyo (bila ya kueleza maradhi
yanayomsumbua mteja wake), alidai mbali na mshitakiwa kuwepo Zanzibar,
ameshindwa kufika mbele ya mahakama hiyo kutokana na sababu za kiafya.
Mayalla aliwasilisha mahakamani hapoi ‘board pass’
pamoja na kipande cha tiketi alichotumia mshitakiwa katika safari yake,
kuthibitisha ukweli wa hoja yake na nia aliyokuwanayo kuhudhuria katika kikao
hicho.
Hata hivyo, ombi la Wakili huyo lilipata upinzani
mkubwa kutoka upande wa mashataka, pale Muendesha mashtaka,Mkaguzi Msaidizi wa
Polisi, Abdulkadir Miraji alipoiomba mahakama kuwa makini na ombi
lililowasilishwa kwani huenda kuna mbinu zimepangwa kumpa fursa mshitakiwa
kutoroka.
Aliiomba mahakama kuzingatia mwenendo wa mshitakiwa
mahakamani hapo ambao alidai unatia mashaka, hivyo kuwepo wasiwasi wa
kutoroka na kuwakosesha watu wengine haki, pale atakakabidhiwa paspoti hiyo.
Akitoa ufafanuzi baada ya kuibuka hoja zinazopingana,
Hakimu Mohammed aliwataka wadhamini wa mshitakiwa kuhakikisha
wanamfikisha mahakamani siku iliopangwa.
Katika shauri hilo, mshatkiwa Ivan Kode ameshtakiwa
kwa kosa la shambulio la kuumiza mwili, kinyume na kifungu cha 247 sheria namba
6 ya 2004, sheria za Zanzibar, ikidaiwa aliwashambulia watu wanne kwa kuwapiga
bastola yenye risasi za chubwi na kuwasababishia maumivu.
No comments:
Post a Comment