tangazo

tangazo

Monday, February 23, 2015

jukumu kubwa la vyuo vya elimu ya juu hapa nchini ni kutoa Taaluma ASEMA BALOZI SEIF



pemba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema kuwa  ni jukumu kubwa  la vyuo vya elimu ya juu hapa nchini ni kutoa Taaluma inayolenga kurahisisha utekelezaji wa mipango ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Jamii kwa ujumla.
Balozi Seif ameeleza hayo katika  mahafali ya kwanza ya chuo cha elimu ya Biashara Pemba, yaliyofanyika katika viwanja vya chuo cha Amali kilichopo Vitongoji  Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema  kwa fikra za kupanua wigo katika kuongeza fani ya teknolojia ni muhimu zaidi kwa vile itasaidia vijana kuweza kuendana na wakati wa sasa wa mabadiliko ya Sayansi na teknolojia.
Amekishauri chuo hicho kuangalia namna ya kujiunga na Taasisi mbali mbali za Kimataifa za Elimu, ili kujiimarisha zaidi pamoja na kupata fursa za kubadilishana uzoefu na utaalamu miongoni mwa walimu na wanafunzi.
Balozi Seif amesema kuwa zipo Taasisi nyingi za kielimu Duniani, ambazo chuo cha Elimu ya Biashara Zanzibar kinaweza kushirikiana nazo, ili kupiga hatua za haraka kitaaluma sambamba na kuliongezea Taifa Wataalamu watakaosaidia taasisi za umma na zaBinafsi.
ameupongeza Uongozi wa chuo cha Elimu ya Biashara kwa uamuzi wake  wa busara, wa kuanzisha kwa mara ya  kwanza chuo Binafsi ambacho Makao Makuu yake yapo Pemba, wakati jamii imezoea kuona Matawi ya vyuo vya elimu ya juu ndio yanayofunguliwa Kisiwani humo.
Amesema kuwa  uamuzi wao umepelekea vijana wengi Kisiwani Pemba kupata fursa za kujiunga na mafunzo ya elimu kwa gharama nafuu, tofauti na ile wanayotoa wakati wanapoamua kufuatia masomo hayo Unguja na Tanzania Bara.
Akisoma Risala ya Chuo cha elimu ya Biashara Pemba Mkuu wa Chuo hicho ndugu Abdulwahab  Said Aboubakar amesema  kuwa, lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho ni kutoa elimu ya Biashara kwa Vijana, `ili waweze kujinasua  katika tatizo la ajira.
amewashukuru washirika wa chuo hicho waliochangia kufanikisha uanzishwaji wake.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara Pemba ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Nd. Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa  kulikuwa na changamoto kubwa  wakati wa uanzishwaji wa chuo hicho likiwemo tatizo la ukosefu wa Majengo.
Mahafali  hayo ya kwanza ya chuo cha elimu ya Biashara Pemba yamejumuisha Wahitimu 133 wa ngazi ya Cheti katika fani Tano, ambazo ni Uhasibu, Usimamizi wa Biashara, Uongozi wa Rasilimali Watu, Manunuzi na Ugavi pamoja na Mawasiliano ya Umma.

No comments:

Post a Comment